Zaidi ya raia elfu 9 wa Kongo DR wakimbilia Angola kutafuta hifadhi
Maelfu ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamekimbilia nchi jirani ya Angola kwenda kuomba hifadhi kutokana na kushtadi machafuko nchini mwao.
Maafisa wa serikali ya Luanda wamesema Wakongamani 9,200 ambapo 1,400 kati yao ni watoto wadogo, wameingia nchini Angola kutafuta hifadhi, kutokana na kushadidi mapigano katika nchi yao.
Serikali ya Angola imeongeza kuwa, raia hawa wapya wa Kongo DR wameingia nchini humo kutafuta hifadhi katika hali ambayo, tayari kuna wenzao zaidi ya 3,200 ambao walikuwa wamewasili hapo awali na kwa sasa wanahifadhiwa katika kituo cha kupokea wakimbizi cha Mussungue.
Aghalabu ya wakimbizi hao wa Kongo DR wanaingia Angola kupitia mkoa wa Lunda Norte ulioko umbali wa kilomita 656 kaskazini mwa mji mkuu, Luanda na wenye mpaka wa pamoja na Kongo DR na Kongo Brazaville.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, serikali ya Angola ilitangaza kufunga mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na kushtadi machafuko katika mkoa wa Kasai, kusini mwa DRC.
Mkoa wa Kasai umekuwa ukishuhudia machafuko tangu Septemba mwaka jana, ambapo watu zaidi ya 400 wameuawa katika machafuko na mapigano kati ya askari usalama na wanamgambo wanaomuunga mkono kiongozi wao wa zamani Kamuina Nsapu, aliyeua na maafisa usalama.