Baadhi ya marais wa Afrika hawataki Machar arejee Sudan Kusini
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa amesema baadhi ya nchi za kanda ya Afrika Mashariki pamoja na Afrika Kusini haziungi mkono wazo la kurejea mjini Juba, kiongozi wa waasi nchini Sudan Kusini, Riek Machar.
David Shearer, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini amesema aghalabu ya viongozi wa Jumuiya ya Kieneo ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) hawataki kabisa Machar aruhusiwe kurejea nchini Sudan Kusini wakisisitiza kuwa, yumkini kurejea kwake kukawasha moto zaidi wa mapigano na machafuko.
Amesema ili kuupatia ufumbuzi mgogori wa kisiasa nchini humo, kuna ulazima wa kuzijumuisha pande zote katika mchakato wa amani, huku akipongeza hatua ya Rais wa zamani wa Botswana, Festus Mogae, ambaye anaongoza timu ya kimataifa ya upatanishi katika mgogoro wa Sudan Kusini pamoja na Nicholas Haysom, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Sudan na Sudan Kusini kwa kumtembelea Machar na kufanya mazungumzo naye hivi karibuni.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Machi, Machar alikashifu mapendekezo ya kikao cha IGAD akisistiza kuwa yalikuwa ya kuvunja moyo. Alisema IGAD inashirikiana na serikali ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini katika kuwapuuza wapinzani wenye silaha nchini humo, na kwamba kikao hicho cha kieneo kilidhihirisha wazi kusambaratika makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka 2015 kwa ajili ya mzozo wa nchi hiyo.
Kabla ya kikao hicho, serikali ya Sudan Kusini ilizitaka nchi za eneo kumtambua Riek Machar, aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo kama gaidi, baada ya askari watiifu kwa kiongozi huyo kuwateka nyara wafanyakazi wawili wa kigeni, na kuitisha kikomboleo ili wawaachie huru.