May 01, 2017 07:31 UTC
  • Wanamgambo 20 wauawa katika mpaka wa Mali na Burkina Faso

Taarifa kutoka nchini Mali zinasema kuwa, zaidi ya wanamgambo 20 wameuawa katika mpaka wa nchi mbili za magharibi mwa Afrika za Mali na Burkina Faso.

Shirika la habari la AFP limevinukuu vikosi vya Ufaransa vikitangaza habari hiyo na kusema kuwa, wanamgambo hao wameuawa katika msitu wa Foulsare karibu na mpaka wa nchi hizo mbili. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mauaji hayo yamefanyika baada ya watu wenye silaha kumuua mwanajeshi mmoja wa Ufaransa mapema mwezi Aprili. Ripoti hiyo imeongeza kuwa, mashambulizi hayo ya wanajeshi wa Ufaransa yamefanyika kutokea angani na ardhini

Wanamgambo wenye silaha, kaskazini mwa Mali

 

Mali imekuwa ikishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya watu wenye silaha licha ya kuweko askari wa kimataifa wa kulinda amani nchini humo. Hata mpaka wa Mali na Burkina Faso nao umekuwa ukishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya watu wenye silaha. Ouagadougou, mji mkuu wa Burkina Faso ulishuhudia mashambulizi kama hayo mwaka jana ambayo yalipelekea makumi ya watu kuuawa.

Dola la kikoloni la Ufaransa limetumia kisingizio cha kupambana na magaidi, kutuma wanajeshi wake wapatao elfu nne nchini Mali chini ya mwavuli wa operesheni ya Barkhane. 

Mali ilikuwa nchi yenye utulivu, lakini mwaka 2012 wanajeshi walifanya mapinduzi na baada ya hapo kukazuka makundi ya watu wenye silaha walioteka maeneo kadhaa ya kaskazini mwa nchi hiyo kabla ya kufurushwa kwenye baadhi ya maeneo hayo.

Tags