Wamorocco waandamana kuwaunga mkono Wapalestina wanaosusia kula
Wananchi wa Morocco wamefanya maandaamano katika mji mkuu wa nchi hiyo Rabat, kuonyesha uungaji mkono wao kwa wafungwa wa Kipalestina ambao wanadhalilishwa katika jela na magereza ya utawala haramu wa Israel.
Sambamba na kuonyesha uungaji mkono wao kwa wafungwa wa Palestina, waandamanaji hao ambao baada ya kuandamana katika barabara za Rabat na kisha kukita kambi nje ya Bunge la nchi hiyo, wameteketeza kwa moto bendera za utawala wa Kizayuni wa Israel kuonyesha ghadhabu zao kwa utawala huo pandikizi.
Wakati huohuo, kundi la wanachuo wa Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza nao wameanza kususia kula, ikiwa ni kuonyesha uungaji mkono wao kwa mamia ya Wapalestina waliosusia kula. Kwa mujibu wa Press TV, wanachuo watano wameapa kutotia kitu mdomoni kwa muda wa siku tano, ili kuonyesha uungaji mkono wao kwa wafungwa wa Palestina wanaopitia mateso ya kila namna katika jela za utawala haramu wa Israel.
Huku hayo yakirifiwa, kijana mmoja wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 30 amefariki dunia kutokana na makali ya njaa, baada ya kujiunga na Wapalestina wanaosusia kula kuwaunga mkono wafungwa Palestina.
Habari zaidi zinasema kuwa, kijana huyo kwa jina Mazan al-Maghrebi, amefariki dunia akiwa nyumbani kwake mjini Ramallah, baada ya kuamua kuwaunga mkono Wapalestina katika kususia kula chakula, licha ya kuwa na ugonjwa wa figo.
Mgomo wa kususia kula Wapalestina zaidi ya 1,600 wakiongozwa na Marwan Al-Barghuthi ambaye anatumikia kifungo cha maisha jela ulianza tarehe 17 Aprili kwa kaulimbiu ya "Uhuru na Heshima" katika magereza yote ya utawala wa Kizayuni.