Wananchi wa Afrika Kusini wasusia kula kuwaunga mkono mateka wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28628-wananchi_wa_afrika_kusini_wasusia_kula_kuwaunga_mkono_mateka_wa_palestina
Wanaharakati, wafungwa wa kisiasa na wananchi wengine wa Afrika Kusini wamesusia kula chakula kuonyesha uungaji mkono wao kwa mateka wa Kipalestina waliosusia kula tangu Aprili 17 wakiwa katika jela na magereza ya utawala haramu wa Israel.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 04, 2017 07:34 UTC
  • Wananchi wa Afrika Kusini wasusia kula kuwaunga mkono mateka wa Palestina

Wanaharakati, wafungwa wa kisiasa na wananchi wengine wa Afrika Kusini wamesusia kula chakula kuonyesha uungaji mkono wao kwa mateka wa Kipalestina waliosusia kula tangu Aprili 17 wakiwa katika jela na magereza ya utawala haramu wa Israel.

Aghalabu ya wanaharakati waliosusia kula chakula kwa masaa 24 nchini Afrika Kusini ni wafungwa wa zamani wa kisiasa wa Kisiwa cha Robben.

Wakfu wa Kathrada umewataka wananchi wengine wa Afrika Kusini kujiunga na vuguvugu hilo la kususia kula chakula na hususan mnamo Mei 15, siku ambayo imetajwa na waungaji mkono wa Wapalestina kote duniani kuwa "Siku ya Kimataifa ya Kutenda". 

Msemaji wa wakfu huo, Zaakirah Vadi amesema: "Tunawaasa wananchi wa Afrika Kusini kushiriki kwa wingi katika kususia chakula Mei 15, siku ambayo pia maandamano makubwa yanatazamiwa kufanyika katika mikoa 9 ya nchi hii ili kuwashinikiza Wabunge wa Afrika Kusini watangaze uungaji mkono wao kwa wafungwa wa Palestina." 

Marehemu Kathrada na Nelson Mandela

Itakumbukwa kuwa, Ahmed Kathrada, mwanaharakati wa mapambano dhidi ya mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini na ambaye alikuwa mpambe wa karibu wa Hayati Nelson Mandela, aliaga dunia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, akiwa na umri wa miaka 87.

Mbali na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza kujiunga na harakati hizo za kususia kula kushinikiza kukomeshwa ukatili dhidi ya mateka wa Palestina, hivi karibu pia wananchi wa Morocco sambamba na kuonyesha uungaji mkono wao kwa wafungwa wa Kipalestina kwa kufanya maandamano mjini Rabat, waliteketeza  moto bendera za utawala wa Kizayuni wa Israel kuonyesha ghadhabu zao kwa utawala huo pandikizi.