Somalia: Tumemuua kiongozi wa al-Shabaab, Shabelle ya Chini
Siku mbili baada ya wanajeshi watatu wa Marekani kuuawa na kujeruhiwa na genge la al-Shabaab katika eneo la Barii, yapata maili 40 magharibi mwa mji wa Mogadishu, serikali ya Somalia imesema imefanikiwa kumuangamiza kamanda mkuu wa kundi hilo la kigaidi na kitakfiri katika eneo la Shabelle ya Chini.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Habari ya Somalia hii leo imesema kuwa, Moalim Osman Abdi Badil, kamanda wa ngazi za juu wa al-Shabaab pamoja na wanamgambo wengine watatu wa genge hilo waliuawa katika makabiliano na jeshi la Somalia eneo la Shabelle ya Chini, Ijumaa iliyopita, siku ambayo makomandoo wa Marekani waliuawa na kujeruhiwa.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kuuawa kwa kamanda huyo mkuu wa al-Shabaab kumeipa nguvu vita dhidi ya ugaidi katika taifa hilo la Pembe ya Afrika.
Hivi karibuni Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo alitoa msamaha wa siku 60 kwa wanamgambo wa al-Shabaab ambao wataweke silaha chini na wajisalimishe.
Genge hilo la kigaidi limekuwa likipata pigo baada ya jingine katika miezi ya hivi karibuni kutoka kwa jeshi la Somalia na askari wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika AMISOM.
Mwezi uliopita, jeshi la Kenya KDF liliwaua wanamgambo 52 wa kundi la hilo la kigaidi katika shambulio lililofanyika kwenye kambi ya genge hilo huko Badhaadhe, eneo la Juba ya Chini, kusini mwa Somalia.