Rais wa Tanzania amfuta kazi waziri Muhongo
Rais John Magufuli wa Tanzania ametangaza kumfuta kazi Waziri wa Nishati na Madini wa nchi hiyo, Sospeter Muhongo kutokana na kuhusika katika kashfa ya mchanga wa dhahabu uliokuwa unasafirishwa nje ya Tanzania.
Sehemu moja ya taarifa ya Ikulu ya Tanzania ambayo nakala yake moja imeifikia Radio Tehran imesema: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli, ametengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo kuanzia leo tarehe 24 Mei, 2017.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu ya Tanzania, nafasi ya Waziri wa Nishati na Madini ya nchi hiyo itajazwa baadaye.
Kabla ya hapo vyombo vya habari vilikuwa vimemnukuu Magufuli akimtaka Profesa Muhongo ajiuzulu kutokana na kushindwa kusimamia suala la mchanga wa dhahabu unaosafirishwa kwenye makontena nje ya Tanzania.
Hatua ya Rais Magufuli ya kumfuta kazi Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania imechukuliwa baada ya kutolewa ripoti ya kamati iliyokuwa ikichunguza suala la mchanga wa dhahabu kwenye makontena.
Kamati hiyo ya wataalamu wa jiolojia na uchambuzi wa kisayansi iliyoundwa Machi 29 mwaka huu, imesema kuwa imebaini kuwepo madini ya kiasi cha kati ya Sh bilioni 829.4 hadi trilioni 1.439 katika makontena yote 277.
Katika hatua nyingine Rais wa Tanzania amevunja Bodi ya wakala wa ukaguzi wa madini Tanzania TMAA na kumsimamisha kazi Mkurugenzi wake kwa kushindwa kutimiza majukumu yake.
Kamati hiyo imegundua kuwa, makontena zaidi ya 200 yaliyokuwa yakichunguzwa, yalikuwa na dhahabu yenye thamani ya zaidi ya shilingi Trilioni moja za Tanzania.