Kenya kutumia jeshi kutegua mabomu ya barabarani
Kenya imetuma wanajeshi katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kwenda kutegua mabomu yaliyotegwa barabarani baada ya watu 20 wakiwemo maafisa 11 kuuawa katika miripuko ya barabarani kwenye eneo hilo.
Aidha maafisa wa polisi wamewakamata washukiwa kadhaa, akiwemo mtu anayesadikiwa kuwa mataalamu wa mabomu, wanaoaminika kutega mabomu ambayo yamekuwa yakiripuka katika eneo hilo kwa muda wa wiki tatu sasa. Inspekta Jenerali wa Polisi Kenya Joseph Boinett amemtaja aliyekamatwa ametambuliwa kama Ahmed Abdi Yare na alikuwa na bunduki aina ya AK-47 na vifaa ya kutegeneza mabomu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ncini Kenya, Mwenda Njoka amesema wanajeshi watashirikiana na maafisa wa polisi katika kuondoa mabomu ya barabarani yaliyotegwa na magaidi wa kundi la kitakfiri la Al Shabab. Amesema kutegua mabomu hayo ni kazi ngumu lakini tayari oparesheni hiyo imeshaanza ili kuhakikisha kuwa watu zaidi hawapotezi maisha.
Wimbi hili la mashambulizi dhidi ya maafisa usalama nchini Kenya linajiri katika hali ambayo, hivi karibuni, Inspekta Jenerali wa Polisi nchini humo alitahadharisha kuwa baadhi ya wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wamepenyeza nchini kwa ajili ya kuvuruga usalama wa taifa, na kuwataka wananchi kuwa macho na kuripoti matukio yoyote wanayohisi yanaweza kuhatarisha usalama kwa vyombo husika.