Polisi ya Ethiopia yatumia nguvu kuwatawanya wapinzani eneo la Oromia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29680-polisi_ya_ethiopia_yatumia_nguvu_kuwatawanya_wapinzani_eneo_la_oromia
Vyombo vya habari nchini Ethiopia vimeripoti kwamba, polisi ya nchi hiyo imetumia nguvu dhidi ya wapinzani eneo la Oromia ambao walikuwa wanaandamana licha ya kutangazwa hali ya hatari na hivyo kuibua wasi wasi eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 28, 2017 03:44 UTC
  • Polisi ya Ethiopia yatumia nguvu kuwatawanya wapinzani eneo la Oromia

Vyombo vya habari nchini Ethiopia vimeripoti kwamba, polisi ya nchi hiyo imetumia nguvu dhidi ya wapinzani eneo la Oromia ambao walikuwa wanaandamana licha ya kutangazwa hali ya hatari na hivyo kuibua wasi wasi eneo hilo.

Habari zinaarifu kufanyika maandamano mapya eneo hilo lililo umbali wa kilometa 100 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa, licha ya kwamba awali serikali ilikuwa imetangaza hali ya hatari. Maandamano hayo ya amani dhidi ya serikali yalianza tangu mwaka 2015 katika kulalamikia ardhi. Wakulima wa Oromia wanaituhumu serikali kwa kutwaa ardhi na kuwakabidhi wawekezaji huku wao wakisalia bila ya ardhi za kuendeshea shughuli zao za kilimo.

Maandamano ya wananchi wa Ethiopia

Kadhalika waandamanaji wanataka kufanyika marekebisho ya kisiasa na kijamii ukiwemo ukomeshwaji wa ukiukaji wa haki za binaadamu, mauaji dhidi ya raia wa kawaida, kamatakamata na ukandamizaji wa kisiasa dhidi ya makundi ya upinzani. Kwa mujibu wa takwimu za mwisho za kamisheni ya haki za binaadamu nchini Ethiopia, maandamano ya wananchi ya mwaka jana yalipelekea kwa akali watu 669 kuuawa, ambapo kati yao watu 462 walikuwa wakazi wa eneo la Oromia. Hii ni katika hali ambayo Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) limetangaza idadi ya watu waliouawa katika maandamano hayo ya mwaka jana kuwa ni 800. Aidha mwanzoni mwa mwezi huu, Umoja wa Mataifa uliitaka serikali ya Ethiopia kuwaachilia huru watu ambao walitiwa nguvuni katika maandamano hayo kuanzia mwaka jana hadi mwaka huu.

Sehemu nyingine ya maandamano

Zeid bin Ra'ad, Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa alitoa kauli hiyo mwishoni mwa safari yake ya siku tatu ya kuitembelea Ethiopia ambapo aliitaka serikali ya Addis Ababa kuwaachilia huru wapinzani hao zaidi ya elfu  26 waliotiwa mbaroni katika maandamano ya kupinga serikali ya nchi hiyo.