Askari wa Somalia, AMISOM waendelea kuwafurusha magaidi wa Al Shabab
Askari wa Jeshi la kitaifa la Somalia (SNA) wakisaidiwa na askari wa Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM Jumamosi walikomboa maeneo kadhaa kusini mwa nchi hiyo.
Waziri wa habari Ugaas Hassan ameliambia shirika la habari la Xinhua kwamba katika oparesheni ya pamoja, askari hao wamefanikiwa kukomboa maeneo kadhaa kaskazini na kusini mwa mji wa Baidoa.
Ushirikiano wa SNA, AMISOM na vikosi vya serikali ya kusini magharibi vimekomboa meneo mengi ya kaskazini na kusini mwa mji wa Baidoa, likiwemo eneo la Gof-gudud, maeneo ambayo yalikuwa yanashikiliwa na wapiganaji wa kigaidi wa Al Shabab katika siku za karibuni.
Mei 9 magaidi wa kundi la Al-Shabaab waliteka eneo la Gof-gudud, takriban kilomita 35 kaskazini mwa eneo la Bay. Aidha waliwaua askari 6 wa Somalia na kuwajeruhi wengine kadhaa kwenye mlipuko wa bomu la kutegwa chini ya ardhi katika eneo hilo.
Umoja wa Afrika umetuma kikosi chake katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Kikosi hicho cha AMISOM kina wanajeshi kutoka Uganda, Kenya, Burundi na Ethiopia. Askari zaidi ya 22 elfu wanaunda kikosi hicho cha AU kwa ajili ya kupambana na kundi la al Shabab huko Somalia.
Ingawa kundi la al Shabab limefurushwa katika miji yote mikubwa na maeneo muhimu ya Somalia, lakini bado lina wanamgambo wake katika baadhi ya vijiji na miji na hufanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia na maafisa wa Serikali.