Wapinzani Burundi: AU imeshindwa kutetea demokrasia
Viongozi wa upinzani nchini Burundi wameukosoa vikali Umoja wa Afrika (AU) kwa kushindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo tangu mwezi Aprili mwaka jana 2015.
Gervais Rufyikiri, mmoja wa viongozi wa upinzani ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Burundi amesema ujumbe wa ngazi za juu wa AU ambao hivi karibuni uliitembelea nchi hiyo, haukuonyesha uwazi na irada ya kisiasa ya kuutatua mzozo huo na kwa msingi huo, ulishindwa kutetea na kulinda demokrasia ya nchi hiyo. Licha ya serikali ya Rais Pierre Nkurunziza kushikilia kuwa haitafanya mazungumzo na wapinzani kwa madai kuwa wanapanga njama ya kuiondoa madarakani serikali yake, lakini Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ambaye aliuongoza ujumbe huo wa AU amesema Rais Yoweri Museveni wa Uganda karibuni hivi ataitisha kikao kingine ambacho kitahudhuriwa na pande zote za kisiasa Burundi kwa shabaha ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo.
Katika hatua nyingine, polisi ya Burundi imemtia mbaroni 'mwanajeshi' wa Rwanda kwa tuhuma za kuwa nchini kwa lengo la kuvuruga zaidi amani. Uhusiano wa nchi mbili hizo jirani umekuwa ukiyumba katika siku za hivi karibuni, tangu baada ya serikali ya Bujumbura kudai kuwa serikali ya Kigali inashirikiana na waasi kwa madhumuni ya kumwondoa madarakani Rais Nkurunziza.
Mtu huyo anayedaiwa kuwa askari wa Rwanda amekamatwa siku moja baada ya polisi kutangaza kuwa, imemtia mbaroni Hugo Haramategeko, mkuu wa chama cha upinzani cha NADEBU katika eneo la Mutakura linalotajwa kuwa na upinzani mkubwa dhidi ya serikali ya Nkurunziza, jijini Bujumbura.
Tangu mwezi April mwaka jana wakati Rais Nkurunziza alipoidhinishwa na chama chake cha CNDD-FDD kugombea urais kwa muhula wa tatu mfululizo katika uchaguzi uliopita, nchi hiyo ndogo ya katikati mwa Afrika imekuwa ikishuhudia machafuko ambayo yamegharimu maisha ya mamia ya watu huku maelfu ya wengine wakiwa wakimbizi ndani na nje ya nchi yao.