Baraza la Usalama lalaani kuuawa askari wa UNAMID huko Darfur, Sudan
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limelaani shambulizi dhidi ya operesheni ya kikosi cha pamoja cha Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa huko Darfur UNAMID.
Nchi wanachama wa baraza hilo zimelaani shambulizi dhidi ya askari wa kulinda amani wa UNAMID lililofanywa na kundi lisilojulikana katika tukio la unyang'anyi wa gari huko Nyala katika jimbo la Darfur Kusini.
Askari mmoja wa Nigeria aliuawa kwenye shambulizi hilo. Mnigeria huyo ni askari wa 64 kupoteza maisha akihudumu chini ya mwavuli wa UNAMID tangu kikosi hicho kipelekewe Darfur mwaka 2007.
UNAMID ina askari 20,000 kutoka nchi 30 duniani ambapo kikosi hicho mwaka jana kiliongozewa muda mwingine wa mwaka mmoja wa kuhudumu nchini Sudan hadi mwisho wa mwezi huu wa Juni wa 2017.

Kikosi cha pamoja cha Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa UNAMID vilitumwa huko Darfur mwaka 2007 kwa lengo la kulinda raia na kurudisha utulivu katika eneo hilo. Umoja wa Mataifa unakisia kuwa zaidi ya watu laki tatu wamepoteza maisha na wengine milioni mbili na laki 6 wakilazimika kuwa wakimbizi kutokana na machafuko ya karibu miaka 13 sasa katika jimbo hilo.