Askari 30 watiwa nguvuni nchini Cameroon kwa kukiuka kanuni za jeshi
Waziri wa Uinzi wa Cameroon ametangaza kuwa askari 30 wa jeshi la nchi hiyo wametiwa nguvuni kwa tuhuma za kufanya maandamano ya kupinga serikali.
Joseph Beti Assomo ametangaza kuwa askari hao 30 wanatuhumiwa kukiuka kanuni za jeshi la nchi hiyo na kufanya maandamano ya kupinga serikali.
Kwa mujibu wa Assomo wanajeshi hao ambao wanashiriki kwenye operesheni za mataifa kadhaa ya eneo za kupambana na kundi la kigaidi na kitakafiri la Boko Haram katika eneo la Ziwa Chad walifanya maandamano wakidai wapatiwe mishahara, bonasi na marupurupu sawa na wanavyopewa askari wa Cameroon wanaohudumu kwenye operesheni za walinda amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Kuhusiana na dai hilo, Waziri wa Ulinzi wa Cameroon amesema, askari wanaohudumu kwenye operesheni za kijeshi za mataifa kadhaa ya eneo ikiwemo Cameroon yenyewe, Nigeria, Niger na Chad wanalipwa mishahara na marupurupu sawa na wanajeshi wengine wa ndani, lakini hali hiyo ni tofauti na askari wa Cameroon wanaohudumu nje ya nchi.
Kama ilivyojiri kuhusiana na askari wa Cameroon, wanajeshi wa Nigeria wanaohudumu kwenye kikosi cha pamoja mataifa kadhaa cha kupambana na kundi la kigaidi la Boko Haram nao pia hivi karibuni wamelalamikia maslahi na mazingira ya kikazi. Hata hivyo hii ni mara ya kwanza ambapo askari wa Cameroon wameamua kuonyesha malalamiko yao hadharani.
Askari wa jeshi la Cameroon wametiwa nguvuni katika hali ambayo hivi karibuni Rais Paul Biya wa nchi hiyo alitangaza kuwa serikali itasikiliza matakwa ya watu na itakuwa tayari kufanya mazungumzo ikiwa matakwa hayo ni ya halali na ya kisheria.../