Makumi watiwa mbaroni Misri kwa kupinga kukabidhiwa Saudia visiwa vya nchi yao
Polisi ya Misri imewatia mbaroni makumi ya watu wanaopinga jaribio la serikali ya nchi hiyo ya kutaka kuipa Saudia visiwa vya nchi yao vya Tiran na Sanafir.
Baada ya bunge la Misri kupitisha muswada wa kujadili suala la kuipa Saudia visiwa hivyo, polisi ya nchi hiyo imewatia nguvuni makumi ya waandamanaji wakiwemo wanaharakati kadhaa wanaopinga hatua hiyo wanayoitaja kuwa ya uhaini. Kwa mujibu wa habari hiyo watu wasiopungua 50 wametiwa mbaroni mapema leo katika kupinga muswada huo ambao ni utangulizi wa kuipa Saudia sehemu ya ardhi ya Misri.
Kadhalika Wamisri wameikosoa serikali ya Rais Abdel Fattah el-Sisi kwa kufanya biashara kwa ardhi ya Misri. Mwezi April mwaka jana, na katika safari ya Mfalme Salman bin Abdulaziz Aal Saud wa Saudia nchini Misri, mfalme huyo alitiliana saini na Rais Abdel Fattah el-Sisi makubaliano ambayo kwa mujibu wake, Cairo inatakiwa iipe Riyadh visiwa vyake viwili vya Tiran na Sanafir, hatua ambayo imezusha upinzani mkubwa wa kila upande nchini humo.
Mbali na maandamano ya vyama na makundi ya kisiasa nchini humo ya kupinga hatua hiyo, mahakama za Misri pia zilitoa hukumu ya kupinga makubaliano hayo ambayo yalitajwa na mahakama hizo kuwa ni uhaini. Hata hivyo serikali ya Cairo ilikata rufaa na baadaye kushinda kesi hiyo. Wamisri wanaukosoa vikali utawala wa kifalme wa Saudia kutokana na nafasi yake mbaya dhidi ya nchi yao ambapo hata mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali ya Rais Muhammad Mursi wa nchi hiyo yaliyopelekea makumi ya raia wa Misri kuuawa, yalisimamiwa na kufadhiliwa kwa fedha nyingi na Saudi Arabia.