Watu 15 wauawa katika hujuma ya al-Shabab mjini Mogadishu, Somalia
Watu wasiopungua 15 wameuawa katika hujuma ya kigaidi huko Mogadishu, mji mkuu wa Somalia huku kundi la kigaidi la al-Shabab likitangaza kuhusika na shambulizi hilo.
Taarifa zinasema gaidi aliyetekeleza hujuma hiyo alikuwa amesheheni mabomu katika gari la kubeba maziwa ambalo alitumia kuingia makao makuu ya wilaya ya Wadajir mjini Mogadishu.
Maafisa wa usalama wanasema idadi ya waliofariki huenda ikaongezeka baada ya watu wengine tisa kujeruhiwa vibaya katika hujuma hiyo. Msemaji wa kundi la kigaidi la al-Shabab Abdiasis Abu Musab amethibitisha kuhusika kundi hilo la kitakfiri na hujuma hiyo.
Siku chache zilizopita pia magaidi wa al-Shabab walivamia hoteli moja mashuhuri mjini Mogadishu na kuwateka nyara watu usiku kabla ya kuua raia wasiopungua 31.

Umoja wa Afrika umetuma kikosi chake cha kulinda amani katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Kikosi hicho cha AMISOM kina wanajeshi kutoka Uganda, Kenya, Burundi na Ethiopia. Askari zaidi ya 22 elfu wanaunda kikosi hicho cha AU kwa ajili ya kupambana na kundi la kigaidi la al-Shabab huko Somalia.
Ingawa kundi la magaidi wa al-Shabab limefurushwa katika miji yote mikubwa na maeneo muhimu ya Somalia, lakini bado wanamgambo wake katika baadhi ya vijiji na miji hufanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia na maafisa wa serikali.