Jun 24, 2017 04:40 UTC
  • Serikali ya Misri yatuhumiwa kuua raia katika vituo vya jeshi

Kituo kimoja cha Kiafrika kimeituhumu serikali ya Misri kuwa inaendelea kuwateka nyara, kuwatesa na kuwaua wapinzani wa kisiasa.

Kituo cha Kiafrika na Kiarabu cha Haki na Uhuru kimesema katika ripoti iliyotolewa jana kwamba, askari usalama wa Misri na askari kanzu wa serikali ya nchi hiyo wangali wanawateka nyara wapinzani wa kisiasa wa serikali wakiwa majumbani au makazini kwao na kuwaua.

Ripoti ya kituo hicho imeitahadharisha serikali ya Cairo kuhusu mauaji ya wapinzani wa kisiasa na raia wa kawaida na kusema: Mauaji ya wapinzani na raia wa kawaida ni ukiukaji wa haki za binadamu na kielelezo kwamba Misri imetumbukia katika janga kubwa la kisheria.

Wapinzani wengi wa kisiasa wanashikiliwa katika jela za Misri

Awali Kamisheni ya Haki na Uhuru ya Misri ilikuwa imesema katika ripoti yake iliyotolewa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kuwatetea Wahanga wa Mateso kwamba, zaidi ya raia wa kawaida 1000 wa Misri waliteswa na kunyanyaswa katika jela za siri zilizoko kwenye kituo cha jeshi cha al Jalaa mkoani Ismailiyya kati ya mwaka 2014 na 2016. Ripoti ya kamisheni hiyo iliyopewa anwani ya: Komesheni Utekaji Nyara wa Raia, imesisitiza kuwa, raia 107 wametoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu tarehe Mosi Januari hadi Machi mwaka huu wa 2017 nchini Misri.  

Tags