Chad: Ikiwa hatutapewa msaada wa fedha, tutajiondoa operesheni za kijeshi Afrika
Rais Idriss Déby wa Chad amesema kuwa, ikiwa nchi hiyo itaendelea kunyimwa pesa za msaada kwa ajili ya kutatua matatizo yake ya kiuchumi na kijamii, basi nayo itajiondoa kushiriki operesheni za kijeshi katika mataifa ya Afrika.
Sambamba na kuashiria mgogoro wa kiuchumi unaoikabili nchi yake Rais Déby amesema kuwa, hadi sasa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika bado hazijawahi kuisaidia nchi hiyo na kwa ajili hiyo ikiwa mwenendo huo utaendelea hivyo basi serikali ya N'Djamena italazimika kujiondoka katika operesheni za kijeshi katika mataifa ya Afrika.
Akizungumzia suala la ushiriki wa Chad katika mafunzo ya kijeshi ya nchi tano za eneo la Sahel mwa Afrika amesema kuwa, Chad haipendelei kushiriki operesheni hizo kwa kuwa haiwezekani katika wakati mmoja iwe na askari 1400 nchini Mali na wakati huo huo itume askari wengine 2000 katika eneo hilo la Sahel. Itafahamika kuwa Chad ni nchi ya tatu kwa kuwa na askari wengi nchini Mali chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa MINUSMA ambapo askari wake 1390 wanashiriki katika operesheni za kulinda amani nchini humo. Mbali na hapo Chad ina askari 2000 wanaoshiriki katika kikosi cha mataifa kadhaa kilichoundwa mwaka 2015. Kikosi hicho kinazijumuisha nchi za Nigeria, Niger, Chad na Cameroon kwa ajili ya kupambana na wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram huko kaskazini mwa Nigeria.
Maeneo ya Sahel yanayoyajumuisha maeneo ya magharibi na mashariki mwa bara hilo ni pamoja na mataifa ya Kaskazini mwa Senegal, kusini mwa Mauritania, katikati mwa Mali, kusini mwa Algeria na Niger, katikati mwa Chad, kusini mwa Sudan, kaskazini mwa Sudan Kusini na Eritrea.