Wamisri wafanya maandamano makubwa kupinga kuipa Saudia visiwa vya nchi yao
Hatua ya Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri ya kutia saini makubaliano ya kuikabidhi Saudi Arabia visiwa viwili vya nchi hiyo vya Tiran na Sanafir, imeibua hasira kubwa baina ya raia wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Kufuatia hatua hiyo, wapinzani wa mpango huo sambamba na kutoa taarifa ya kuwataka raia wote wa Misri kushiriki katika maandamano makubwa siku ya Iddul-Fitri iliyoswaliwa Jumapili ya jana nchini humo, wamefanya maandamano hayo katika kuonyesha umuhimu wa kulindwa kila shibri ya ardhi ya nchi yao.
Katika maandamano hayo, raia wa Misri wametia saini hati ya kupinga hatua hiyo ambapo wameitaka serikali ya Cairo kubatilisha haraka makubaliano ya kuiuza sehemu ya ardhi ya nchi hiyo Saudia. Baada ya bunge la Misri kupasisha mpango wa kuchorwa upya mipaka ya baharini ya nchi hiyo na Saudia, Jumamosi iliyopita, Rais Abdel Fattah el-Sisi alitia saini makubaliano hayo ambayo ni mwanzo wa kuikabidhi Riyadh sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Hatua ya bunge la Misri ya kupitisha muswada huo hapo tarehe 14 Juni 2017, ilizusha malalamiko makubwa kati ya watu wa matabaka tofauti ya Misri. Wapinzani wanamtuhumu Rais Abdel Fattah el-Sisi kwa uhaini kutokana na hatua yake ya kuipa Saudia visiwa vya nchi hiyo baada ya kupewa mamilioni ya Dola na Mfalme Salman bin Abdulaziz Aal Saud.
Mwezi Aprili mwaka jana, na katika safari ya Mfalme Salman bin Abdulaziz Aal Saud wa Saudia nchini Misri, mfalme huyo alitiliana saini na Rais Abdel Fattah el-Sisi makubaliano ambayo yanaiwajibisha Cairo kuipa Riyadh visiwa vyake viwili vya Tiran na Sanafir, hatua ambayo imezusha upinzani mkubwa nchini humo.