Mkutano wa 29 wa Umoja wa Afrika wamalizika mjini Addis Ababa Ethiopia
Mkutano wa 29 wa kilele wa Umoja wa Afrika uliokuwa ukifanyika katika makao makuu ya umoja huo huko Addis Ababa Ethiopia, umemalizika huku wakuu wa nchi wanachama wakisisitiza juu ya kupatiwa ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazolikabili bara hilo.
Mkutano huo umesema kuwa, nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zitaimarisha ushirikiano wa kikanda na wa kimataifa ili kukabiliana kwa pamoja na changamoto za usalama ambazo zinazikabili nchi mbalimbali za bara la Afrika.
Kutokana na hali ngumu ya usalama barani Afrika, amani na usalama ilikuwa ajenda muhimu ya mkutano huo. Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahmat amesisitiza kuwa, amani na usalama ni msingi wa maendeleo ya uchumi wa nchi za Afrika, na suala la amani na usalama pia ni changamoto kubwa kabisa inayoukabili Umoja wa Afrika.
Amesema kuwa, kuna haja ya kuchukuliwa hatua za maana ili kukabiliana na changamoto hizo.
Aidha Moussa Faki Mahmat amezikosoa nchi wanachama wa Umoja huo kwa kushindwa kuonesha mshikamano kwa nchi zinazokabiliwa na janga la njaa barani humo.
Imeelezwea kuwa, mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika mara hii ulijikita zaidi katika ajenda ya jinsi gani ya kuweza kufanya mageuzi ndani ya umoja huo pamoja na kuuwezesha kutotegemea ufadhili kutoka nje.
Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe alichangia dola milioni moja kwenye Umoja wa Afrika akilenga kuonyesha mfano kwa nchi za Afrika ili kufadhili shughuli za Umoja huo na kuachana na misaada kutoka kwa wafadhili.