Mkuu wa Polisi Tanzania kuzungumzia mauaji ya mkoani Pwani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31374-mkuu_wa_polisi_tanzania_kuzungumzia_mauaji_ya_mkoani_pwani
Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania, Simon Sirro amesema hivi karibuni atazungumza kuhusu suala la mauaji yanayotokea mkoani Pwani.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jul 05, 2017 10:05 UTC
  • Mkuu wa Polisi Tanzania kuzungumzia mauaji ya mkoani Pwani

Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania, Simon Sirro amesema hivi karibuni atazungumza kuhusu suala la mauaji yanayotokea mkoani Pwani.

Akizungumza leo mjini Dar es Salaam, IGP Sirro ameongeza kuwa, Watanzania hawajazoea mambo ya fujo fujo na kwamba wale waliotumwa kwa ubaya watajibiwa vikali.

Watu takribani 37 wamepoteza maisha tangu Mei mwaka jana yalipoibuka mauaji ya kutumia risasi katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani. Kati ya waliouawa katika hujuma hizi ni askari wa polisi na viongozi wa serikali za mitaa.

Maafisa wa Polisi Tanzania

Jeshi la Polisi Tanzania hivi karibuni lilitangaza kuunda Kanda Maalumu ya Rufiji ili kukabiliana na mauaji katika eneo hilo. Aidha jeshi hilo limesema limeua watu wanne wanaosadikiwa kuwa miongoni mwa wauaji na kutangaza majina yawengine 16 linaowasaka kwa tuhuma za kuendesha vitendo hivyo. Aidha IGP Sirro ametoa wito kwa wananchi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa kamanda mpya wa Kanda Maalumu ya Rufiji ili kuhakikisha mauaji hayo yanakwisha.