Amnesty International: EU inapaswa kubeba jukumu la wahamiaji wa Libya
Shirika la Msamaha la Kimataifa (Amnesty International) limesema kuwa, Umoja wa Ulaya (EU) unapaswa kubeba lawama za hali mbaya ya wahajiri nchini Libya.
Shirika la habari la IRIB limenukuu taarifa ya shirika hilo ikisema kuwa, nchi hizo za Ulaya si tu zimeshindwa kuchukua hatua yoyote ya kuwasaidia wahajiri hao lakini pia zimeweka sheria kali ambazo zinakwamisha kazi za jumuiya na taasisi zisizo za kiserikali za misaada ya kibinadamu.
Taarifa ya Shirika la Amnesty International katika masuala ya haki za binadamu imeongeza kuwa, kila wiki wahajiri kadhaa wanapoteza maisha nchini Libya kutokana na nchi za Ulaya kukataa kutoa ushirikiano unaotakiwa wa kuwasaidia wahajiri hao. Shirika hilo limeutaka Umoja wa Ulaya kufungua njia nyingi za kisheria kwa ajili ya wahajiri hao ili waweze kuingia barani Ulaya kwa njia za salama na amani kamili.
Mwaka uliopita wa 2016 ulikuwa mwaka wa maafa makubwa zaidi kwa wahajiri wanaotumia bahari ya Mediterranean kukimbilia Ulaya. Tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa pia, zaidi ya wahajiri 2000 wa Libya wamepoteza maisha katika jitihada za kuingia barani Ulaya kinyume cha sheria.
Tangu mwaka 2015 hadi hivi sasa, bara Ulaya limevamiwa na wimbi kubwa la mamia ya maelfu ya wahajiri ambao wanakimbia nchi zao kutokana na sababu mbalimbali hasa migogoro ya kisiasa inayochochewa na nchi za Magharibi na Marekani pamoja na waitifaki wao kama vile Saudi Arabia na Uturuki. Watu hao wanalazimika kukimbilia Ulaya kutafuta usalama baada ya maeneo yao kuvamiwa na magenge ya kigaidi yanayoungwa mkono na nchi za Ulaya, Marekani na waitifaki wao.