Misri yashutumiwa kwa kuwatia mbaroni makumi ya wanachuo wa kigeni
Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Human Rights Watch limeishutumu Misri kwa kuwatia mbaroni makumi ya wanachuo Waislamu kutoka China.
Mkurugenzi wa kitengo cha Mashariki ya Kati cha shirika la Human Rights Watch, Bi Sarah Leah Whitson ameandika katika ukurasa wake wa Tweeter kwamba "Misri imewatia mbaroni kwa namna ya kusikitisha, wanachuo Waislamu kutoka China na inaonekana imefanya hivyo kwa maombi ya viongozi wa China."
Whitson ameongeza kuwa, ni jukumu la serikali ya Misri kuwapa wakili wa kuwatetea makumi ya wanafunzi hao wa vyuo vikuu kutoka China.
Amesema, Human Rights Watch ina wasiwasi mkubwa wa kuteswa na kufanyiwa vitendo visivyo vya kibinadamu wanachuo hao wa China katika korokoro za Misri.
Wanachuo na wanaharakati wa jamii ya Uyghur ya China wamesema kuwa, siku ya Jumanne, polisi wa Misri waliivamia mikahawa inayoendeshwa na jamii ya Uyghur mjini Cairo na kuwatia mbaroni wanachuo 30 Waislamu, raia wa China.
Sehemu kubwa ya jamii ya Uyghur ni Waislamu wanaozungumza lugha ya Kituruki. Baadhi ya watu ya jamii hiyo wanailaumu serikali ya China kwa kukandamiza utamaduni na imani ya kidini ya watu wa jamii hiyo.