Wapinzani Madagascar wafanya maandamano licha ya marufuku ya polisi
Wafuasi wa kambi ya upinzani nchini Madagascar wamefanya maandamano leo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Antananarivo licha ya maandamano hayo kupigwa marufuku na vyombo vya usalama.
Maandamano hayo yameitishwa na chama cha rais wa zamani wa Madagascar, Marc Ravalomanana kwa kile kilichotajwa ni kuadhimisha mwaka wa 15 tangu chama hicho kilipoundwa.
Polisi ya Madagascar imekabiliana na maandamano hayo na kutawanya waandamanaji kwa kutumia gesi ya kutoa machozi. Polisi inasema, maandamano hayo yameitishwa kinyume cha sheria.
Ravalomanana alishika madaraka ya Madagascar mwaka 2002 na mwaka 2009 aliondolewa madarakani na aliyekuwa meya wa mji mkuu wa nchi hiyo, Andry Rajoelina, suala ambalo liliitumbukiza nchi hiyo katika machafuko ya ndani yaliyoendelea kwa miaka kadhaa.
Katika wiki za hivi karibuni nchi hiyo imekuwa ikisumbuliwa na machafuko na ghasia za kisiasa. Wapinzani wa Rais Hery Rajaonarimampianina wa nchi hiyo wanamtuhumu kwamba, anazishinikiza mahakama za nchi hiyo kwa maslahi ya washauri na jamaa zake wa karibu wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi na kupora mali ya umma.