UN: Elfu 80 mashariki mwa Congo walazimika kukimbia vita na machafuko
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, watu wapatao elfu 80 wamekimbia makazi yao huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na vita na mapigano yanayoendelea kati ya jeshi la serikali ya nchi hiyo na muungano mpya wa makundi ya waasi.
Mapigano hayo yanafanyika katika eneo la Fizi kwenye mkoa wa Kivu Kusini baina ya muungano wa waasi wa National Coalition of the People for the Sovereignty of Congo (CNPSC) na jeshi la Congo DR.
Mwezi uliopita waasi hao waliteka miji kadhaa ya eneo hilo kabla ya kuzidiwa nguvu na jeshi la serikali ya Kinshasa na ripoti zinasema zaidi ya watu 10 waliuawa.
Zaidi ya raia milioni moja na nusu wamekimbia makazi na nyumba zao katika maeneo ya mashariki mwa Congo mwaka huu pekee kutokana na machafuko yanayoendelea katika eneo hilo. Watu wengine 3000 wamepoteza maisha tangu mwezi Oktoba mwaka jana katika eneo hilo katika machafuko ya kupinga seikali ya Rais Joseph Kabila wa Congo.