FAO yatahadharisha kuhusu njaa Afrika Mashariki
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31832-fao_yatahadharisha_kuhusu_njaa_afrika_mashariki
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO limetahadahrisha kuwa ukosefu wa mvua Afrika Mashariki umeongeza njaa katika eneo hilo.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Jul 16, 2017 02:15 UTC
  • FAO yatahadharisha kuhusu njaa Afrika Mashariki

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO limetahadahrisha kuwa ukosefu wa mvua Afrika Mashariki umeongeza njaa katika eneo hilo.

Katika taarifa FAO imesema hali hiyo imepelekea mazao kuangamia, jamii kukosa lishe bora, na maelfu ya mifugo kufa na kwamba wafugaji wamebeba mzigo mkubwa wa ukosefu huo wa mvua.

Tahadhari hiyo imeonya kwamba mfululizo wa tatu wa ukosefu wa mvua za msimu umeathiri zaidi Somalia kusini na kati, kusini mashariki mwa Ethiopia, kaskazini na mashariki mwa Kenya, kaskazini mwa Tanzania pamoja na kaskazini mashariki na magharibi mwa Uganda, ambako watu wamepoteza uwezo wao huku wakiwa hawana njia mbadala za kukabiliana na baa hili.

FAO imesema idadi ya watu wanaohitaji msaada wa dharura wa kibinadamu katika maeneo hayo, ambayo sasa inakadiriwa kuwa milioni 16, imeongezeka kwa asilimia 30 tangu mwishoni mwa mwaka 2016 na iwapo msaada wa haraka hautatolewa basi hali yao itakuwa mbaya zaidi kwani msimu wa kiangazi unawadia katika miezi michache ijayo.

Taarifa hiyo pia imesema mavuno yamepungua katika maeneo ya kati, kusini mashariki na pwani mwa Kenya. Katika nchi jirani ya Tanzania upungufu wa mvua umetabiriwa kupunguza mazao ya mahindi katika maeneo ya kaskazini na kati huku maeneo ya kusini maghairbi na kaskaizni mwa Uganda nayo yakiwa na hali mbaya ya chakula.