Marais wa Tanzania na Burundi wawataka Warundi kurudi kwao, wasema kuna amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32048-marais_wa_tanzania_na_burundi_wawataka_warundi_kurudi_kwao_wasema_kuna_amani
Marais John Pombe Magufuli wa Tanzania na Pierre Nkurunziza wa Burundi kwa pamoja wamewataka raia wa Burundi waliokimbilia Tanzania, kurudi kwao kwa hiari. Marais hao yametoa kauli hiyo Alkhamisi ya jana mji wa Ngara, mkoa wa Kagera nchini Tanzania.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 20, 2017 23:01 UTC
  • Marais wa Tanzania na Burundi wawataka Warundi kurudi kwao, wasema kuna amani

Marais John Pombe Magufuli wa Tanzania na Pierre Nkurunziza wa Burundi kwa pamoja wamewataka raia wa Burundi waliokimbilia Tanzania, kurudi kwao kwa hiari. Marais hao yametoa kauli hiyo Alkhamisi ya jana mji wa Ngara, mkoa wa Kagera nchini Tanzania.

Katika  mkutano huo marais hao mbali na kuzungumza na wananchi, wamefanya pia mazungumzo ya kuimarisha mahusiano ya pande mbili hususan katika uga wa usalama na biashara. Awali akizungumza na Warundi waliokuwa wamefika katika mkutano huo, Rais Perre Nkurunziza aliwataka raia wa nchi yake ya Burundi kurudi nyumbani na kusisitiza kuwa, hivi sasa Burundi ina amani ya kutosha. Aidha ametoa shukurani nyingi kwa Tanzania kwa kuwapokea Warundi katika kipindi cha shida na kuongeza kuwa, Tanzania na Burundi ni mataifa rafiki.

Wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania

Kwa upande wake Rais Magufuli amesema kuwa, sasa umefika wakati wa Warundi kurundi nyumbani kwa hiari ili wakajenge nchi yao. Pia ameyataka mashirika yanayoshughulikia wakimbizi kuacha kuwatisha raia hao wa Burundi kwamba bado nchi yao ina machafuko na badala yake yajikite kutangaza amani. Amesisitiza kuwa, Tanzania haiwafukuzi ila wanatakiwa kurudi nchini kwao kwa hiari. Katika sehemu nyingine Rais Magufuli amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo, Mwigulu Nchemba kusimamisha kuwapa uraia raia wa Burundi kuanzia sasa.

Hali ya mchafukoge nchini Burundi

Kwa mujibu wa Waziri Nchemba, katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2017, Tanzania iliwapa uraia wakimbizi wa Burundi wapatao 1060. Alidha alisema kuwa, kati ya wakimbizi 247,000 waliopo nchini humo 5,000 wameomba kurudi kwao kwa hiari.