Wamorocco waendeleza maandamano Al Hoceima, polisi 72 wajeruhiwa
Maandamano ya wakazi wa mji wa Al Hoceima, kaskazini mwa Morocco yameendelea huku askari 72 wakijeruhiwa.
Licha ya serikali kuwataka wakazi wa mji wa Al Hoceima kukukomesha maandamano, lakini mamia ya watu usiku uliopita walimiminika mabarabarani katika maandamano ya kuitaka serikali iwaachilia huru watu inaowashikilia na vyombo vya usalama. Katika maandamano hayo kundi moja la watu waliokuwa wamefunika nyuso zao liliwashambulia maafisa usalama 72, huku polisi nao wakipiga mabomu ya kutoa machozi katika kujaribu kuwatawanya.
Kufuatia hali hiyo waandamanaji 11 walizimia kutokana na kukosa pumzi na kupelekwa hospitali. Vilevile magari mawili ya polisi yamechomwa moto na waandamanaji. Yapata miezi minane sasa ambapo raia wa Morocco wamekuwa wakiandamana dhidi ya serikali ya Rabat. Maandamano nchini Morocco yalianza baada ya muuza samaki Mouhcine Fikri kubinywabinywa na kufa ndani ya lori la kuzoa takataka katika mji wa kaskazini mwa nchi hiyo wa Al Hoceima akijaribu kuchukua samaki wake waliotupwa humo na polisi.
Katika kipindi hicho raia wa taifa hilo walikuwa wakifanya maandamano ya amani kutaka serikali itekeleze uadilifu dhidi ya wahusika wa jinai hiyo. Mouhcine Fikri alikuwa amenunua sakamaki wake bandarini kabla ya kupokonywa na polisi baada ya wakuu wa eneo hilo kupiga marufuku uuzaji wa baadhi ya samaki.