Misri yawahukumu maisha jela wanaharakati 43 wa Ikhwani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32260-misri_yawahukumu_maisha_jela_wanaharakati_43_wa_ikhwani
Mahakama ya Jinai ya Misri imewahukumu wanaharakati 43 wa harakati ya Ikhwanul Muslimin kifungo cha maisha jela kwa madai kwamba wamepatikana na hatia ya kushiriki maandamano dhidi ya serikali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 25, 2017 22:38 UTC
  • Misri yawahukumu maisha jela wanaharakati 43 wa Ikhwani

Mahakama ya Jinai ya Misri imewahukumu wanaharakati 43 wa harakati ya Ikhwanul Muslimin kifungo cha maisha jela kwa madai kwamba wamepatikana na hatia ya kushiriki maandamano dhidi ya serikali.

Katika hukumu hiyo ya jana Jumanne, mahakama hiyo imesema wanaharakati hao walishiriki maandamano yaliyopigwa marufuku dhidi ya serikali, kuwashambulia maafisa usalama na kupora mali za umma wakati wa maandamano hayo mwezi Disemba mwaka 2011.

Mbali na kuwahukumu kifungo cha maisha jela, mahakama hiyo imewapiga faini washtakiwa hao ya dola 948,661 za Marekani eti kwa kupora mali za umma.

Wanaharakati wengine 9 wa Ikhwani wamehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela huku 92 wakiachiwa huru.

Wanaharakati wakifuatilia kesi zao mahakamani Misri

Baada ya jeshi la Misri kumuondoa madarakani Muhammad Mursi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin hapo mwaka 2013, serikali ya Cairo ilipiga marufuku shughuli zote za harakati hiyo.

Kadhalika idadi kubwa ya viongozi na wanachama wa harakati hiyo iliyopigwa marufuku wamefungwa jela na baadhi yao wamehukumiwa adhabu ya kifo.