Ugonjwa wa Hepatitis B unaongoza kwa kuuwa Watanzania kuliko Ukimwi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32384-ugonjwa_wa_hepatitis_b_unaongoza_kwa_kuuwa_watanzania_kuliko_ukimwi
Serikali ya Tanzania imesema kuwa, maambukizi ya ugonjwa wa Homa ya Ini au Hepatitis B, yameongezeka mara mbili yakilinganishwa na Virusi vya Ukimwi HIV nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 28, 2017 09:38 UTC
  • Ugonjwa wa Hepatitis B unaongoza kwa kuuwa Watanzania kuliko Ukimwi

Serikali ya Tanzania imesema kuwa, maambukizi ya ugonjwa wa Homa ya Ini au Hepatitis B, yameongezeka mara mbili yakilinganishwa na Virusi vya Ukimwi HIV nchini humo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akizungumza na vyombo vya habari leo Ijumaa na kuongeza kuwa, ugonjwa wa Homa ya Ini (Hepatitis B) unaongoza kwa kuua Watanzania kutokana na maambukizi yake kufikia asilimia 16, huku virusi vya ugonjwa wa Ukimwi, ikiwa ni asilimia 5.3.

Ugonjwa wa Hepatitis-B unavyoshambulia ini

Aidha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini Tanzania amesema kuwa, ugonjwa huo huua taratibu ukilinganishwa na magonjwa mengine kwa kuwa dalili zake huchukua muda mrefu kuweza kujulikana na kujitokeza wazi kwa mgonjwa. Amesema licha ya kwamba mpaka sasa hakuna takwimu halisi za wagonjwa wa maradhi hayo kutokana na watu kutokuwa na tabia za kupima afya zao, idadi ya wagonjwa wanaobainika kuwa na homa hiyo wengi huwa wamefikia hatua za mwisho za ugonjwa huo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu

Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa, mara nyingi wizara yake huwa inapata takwimu hizo kupitia uchangiaji wa damu, ambapo damu inayokutwa na ugonjwa wa Homa ya Ini huwa ni nyingi zaidi ikilinganishwa na ile yenye Virusi vya Ukimwi. Kufuatia hali hiyo, amewataka Watanzania kuwa na mazowea ya kupima afya zao mara kwa mara ili kubaini hali ya muhusika mapema zaidi kabla ya ugonjwa kuwa umefikia hatua isiyoweza kuzuilika.