Mipaka ya Libya na Tunisia yatajwa kuwa maficho ya wanachama wa Daesh
Mipaka ya Libya na Tunisia imetajwa kuwa maficho ya wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh.
Mtandao wa habari wa Libya 24 umetoa taarifa kuhusiana na harakati za kundi la kigaidi la Daesh huko kaskazini mwa Afrika na kuandika kuwa, hivi sasa mamia ya wanachama wa kundi hilo ambao wamekuwa wakifanya jinai nchini Libya wanajikusanya katika maeneo ya mipaka ya nchi hizo mbili. Mtandao huo wa habari umefafanua kuwa, maeneo hayo yamegeuka na kuwa maficho ya magaidi hao. Limefichua kuwa, kutokana na kundi hilo kupoteza maeneo yake mengi lililokuwa linayadhibiti huko Syria na Iraq, sasa wanachama wake wanajikusanya nchini Libya hasa kutokana na hali ya machafuko yanayotawala nchi hiyo.
Mtandao huo wa habari umelinukuu jeshi la Libya likisema kwamba, tangu mwaka 2013 yaani kabla hata ya kudhibiti baadhi ya maeneo ya Iraq, kundi hilo la kigaidi lilikuwa tayari limeanzisha harakati zake ndani ya ardhi za Libya.
Weledi wa mambo wanaamini kwamba, kundi la Daesh linajiandaa kufanya mashambulizi makali katika taasisi za mafuta na bandari za Libya mashambulizi ambayo yatazidisha hofu na wasiwasi kwa raia wa nchi hiyo na kuwafanya wakimbizi katika nchi jirani na zile za Ulaya.