Al-Shabaab washadidisha hujuma kabla ya uchaguzi, waua watu 4 Kenya
Huku uchaguzi mkuu wa Agosti 8 ukizidi kujongea nchini Kenya, kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab linaonekana kushadidisha mashambulizi yake dhidi ya raia na maafisa usalama wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Afisa mmoja wa polisi ya Kenya ameuawa usiku wa kuamkia leo baada ya magaidi hao kuvamia makao makuu ya kaunti ndogo ya Lafey katika jimbo la Mandera kaskazini mashariki mwa nchi.
Frederick Shisia, Kamishna wa Kaunti ya Mandera amesema wanachama wapatao 50 wa genge la al-Shabaab wameshambulia makao makuu ya kaunti hiyo pamoja na kambi ya Polisi ya Utawala katika eneo hilo mwendo wa saa nane usiku wa jana.
Naye Eric Oronyi, Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Lafey amesema kwa akali magaidi watatu wa al-Shabaab wameuawa katika makabiliano ya risasi na maafisa usalama wa eneo hilo, na kwamba matakfiri hao wamechoma moto magari matatu ya serikali.
Hii ni katika hali ambayo, watu watatu waliripotiwa kuuawa jana adhuhuri baada ya wanachama wengine wa al-Shabaab kushambulia basi la abiria katika kaunti ya Lamu.
Mkuu wa Polisi katika eneo la Pwani, Larry Kieng amesema basi hilo lilikuwa linatoka Mombasa kuelekea Kipini wakati liliposhambuliwa na magaidi kwa kumiminiwa risasi.
Hali hii inashuhudiwa nchini Kenya ikiwa zimesalia siku chache hadi kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo.