Magaidi wa al-Shabaab wateka na kudhibiti mji kusini mwa Somalia
Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab la Somalia limetangaza kuwa limeuteka na kuudhibiti mji wa Leego, ulioko kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Mji huo uko umbali wa kilomita 130 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu, eneo la Shabelle ya Chini.
Siku chache zilizopita, Jeshi la Uganda lilitangaza habari ya kuuawa askari 12 wa nchi hiyo katika shambulizi la al-Shabaab katika eneo hilo.
Kadhalika askari wengine saba wa UPDF ambao walikuwa sehemu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) walijeruhiwa katika shambulio hilo.
Naibu Gavana wa mkoa wa Lower Shabelle, Ali Nur alisema kuwa askari 23 wa kikosi cha AMISOM na mmoja wa jeshi la Somalia wameuwa katika shambulizi hilo la kuvizia la al-Shabaab.
Haijabainika iwapo vikosi hivyo vya AMISOM na Jeshi la Somalia vimeondoka katika mji wa Leego kutokana na hujuma hiyo ya al-Shabaab ya wiki iliyopita.
AbdiAziz Abu Musab, msemaji wa operesheni za kijeshi za al-Shabaab alidai kuwa, kundi hilo la kigaidi limeua wanajeshi 39 wa AMISOM akiwemo kamanda wao katika shambulizi hilo.