KDF yashambulia ngome za al-Shabaab karibu na Afmadow, Somalia
(last modified Thu, 10 Aug 2017 14:45:44 GMT )
Aug 10, 2017 14:45 UTC
  • KDF yashambulia ngome za al-Shabaab karibu na Afmadow, Somalia

Ndege za Jeshi la Ulinzi la Kenya KDF zimeshambulia ngome za kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika eneo la Weelmarow karibu na wilaya ya Afmadow, eneo la Lower Juba, kusini mwa Somalia.

Duru za habari zinasema kuwa ndege hizo za jeshi la Kenya ambazo ni sehemu ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) zilishambulia ngome hizo za al-Shabaab usiku wa kuamkia leo.

Hata hivyo KDF haijatoa maelezo kuhusu hujuma hiyo au idadi ya wanachama wa genge hilo la kigaidi waliouawa na kujeruhiwa. 

Haya yanajiri siku chache baada ya askari 12 wa Jeshi la Ulinzi la Ugada UPDF kuuawa katika shambulizi lililofanywa na wapiganaji wa kundi la kigaidi la al Shabab kusini mwa Somalia. 

Naibu Gavana wa Mkoa wa Lower Shabelle, Ali Nur alisema kuwa askari 23 wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM wakiwemo hao 12 wa Uganda na mmoja wa jeshi la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika waliuawa katika shambulizi hilo la kuvizia la al-Shabab.

Wanachama wa al-Shabaab, Somalia

Hata hivyo al-Shabaab kupitia AbdiAziz Abu Musab, msemaji wa operesheni za kijeshi za genge hilo ilidai kuwa, kundi hilo la ukufurishaji limeua wanajeshi 39 wa AMISOM akiwemo kamanda wao katika shambulizi hilo.

Mapema mwezi huu, kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab lenye mfungamano la mtandao wa al-Qaeda lilitangaza kuwa limeuteka na kuudhibiti mji wa Leego, ulioko kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, umbali wa kilomita 130 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu.

Tags