Kamanda wa zamani al-Shabaab ajiunga na serikali ya Somalia
(last modified Mon, 14 Aug 2017 03:36:22 GMT )
Aug 14, 2017 03:36 UTC
  • Kamanda wa zamani al-Shabaab ajiunga na serikali ya Somalia

Aliyekuwa Naibu Kiongozi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab na pia msemaji wa zamani wa genge hilo la ukufurishaji Mukhtar Robow Abu Mansur, amejisalimisha kwa jeshi la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Kanali Nur Mohamed, askari wa jeshi la Somalia amesema Robow amejisalimisha kwa jeshi la nchi hiyo katika mji wa Hudur, kusini magharibi mwa nchi na kwamba karibuni hivi atasafirishwa kwa ndege hadi mji mkuu Mogadishu kukutana na maafisa wa serikali.

Hata hivyo hajatoa ufafanuzi kuhusu jambo lililompelekea kinara huyo wa zamani wa al-Shabaab kuamua kujisalimisha kwa vyombo vya dola.

Baadhi ya duru za habari zinasema, yumkini Robow amejiunga na serikali na kuacha harakati za kigaidi baada ya Marekani kuondoa jina lake katika orodha ya magaidi hatari inayowasaka miezi miwili iliyopita.

Marekani ilimuondoa Robow katika orodha hiyo baada ya miaka mitano sambamba na kufuta zawadi ya Dola milioni 5 kwa yeyote angemkamata au angetoa taarifa ya kupelekea kukamatwa kwake.

Mukhtar Robow Abu Mansur, msemaji wa zamani wa al-Shabaab

Wiki iliyopita, mapigano makali kati ya wanachama wa kundi hilo la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabab na wapiganaji watiifu kwa Mukhtaar Robow, kinara wa zamani wa kundi hilo huko kusini magharibi mwa Somalia yalipelekea kwa akali watu 20 kuuawa na wengine kujeruhiwa.

Mohamed Aden, mhadhiri wa somo la Historia katika Chuo Kikuu cha Mogadishu ametilia shaka hatua ya serikali ya Mogadishu kumpokea Robow na kusema kuwa, iwapo magaidi walioweka silaha chini na kujisalimisha hawatapandishwa kizimbani kutokana na jinai walizozifanya huko nyuma, basi ni muhali Somalia ishuhudie amani.

 

 

 

Tags