Serikali ya Somalia yayaonya mashirika na taasisi za fedha zinazoisaidia al Shabab
Serikali ya Somalia imayaonya mashirika na taasisi za mawasiliano na za kifedha zinazohusika na usafirishaji wa fedha kwa ajili ya kundi la kigaidi na kiwahabi la al Shabab nchini humo.
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Somalia, Mohammed Abubakar Ayslav, aliyasema hayo Jumapili ya jana ambapo sambamba na kubainisha kuwa baadhi ya mashirika yanasaidia kusafirisha fedha za kundi hilo la kigaidi alisema kuwa, serikali ya Mogadishu imeyapiga marufuku mashirika ya huduma za mawadiliano na uhamishaji fedha kushirikiana na kundi hilo. Ameongeza kuwa, benki na mashirika ya usafirishaji wa fedha yatakayokiuka sheria hiyo, yatakabiliwa na adhabu kali.
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Somalia pia ameyataka mashirika hayo kuacha kulipa fedha kwa kundi hilo kwa namna yoyote ile na kwamba kinyume na hivyo yatafuatiliwa kisheria.
Kundi la al Shabab lilitimuliwa kutoka mjini Mogadishu mwezi Agosti 2011 kutokana na kushtadi mashambulizi ya jeshi la Somalia na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika AMISOM. Hata hivyo limekuwa likifanya hujuma za kigaidi kuwalenga askari, maafisa wa serikali na raia wa kawaida katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.