Maporomoko ya udongo yaua watu 40 kaskazini mashariki mwa Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33272-maporomoko_ya_udongo_yaua_watu_40_kaskazini_mashariki_mwa_kongo_dr
Watu 40 wamefariki dunia baada ya maporomoko ya udongo kusomba kijiji kimoja cha uvuvi kwenye fukwe za Ziwa Albert kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 17, 2017 10:07 UTC
  • Maporomoko ya udongo yaua watu 40 kaskazini mashariki mwa Kongo DR

Watu 40 wamefariki dunia baada ya maporomoko ya udongo kusomba kijiji kimoja cha uvuvi kwenye fukwe za Ziwa Albert kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Naibu Gavana wa mkoa wa Ituri Pacifique Keta amesema leo kuwa sehemu moja ya mlima iliimeza kambi moja ya wavuvi baada ya mvua kali kusababisha maporomoko ya udongo. Ameongeza kuwa watu 40 walifariki katika janga hilo lililotokea jana kwenye kijiji cha Tora kilichoko kwenye fukwe za Ziwa Albert.

Kwa mujibu wa Keta, maiti 28 za watu waliofariki katika tukio hilo zilizikwa jana hiyohiyo na nyengine 12 zilitazamiwa kuzikwa leo.

Daktari mmoja katika hospitali ya Tshomia iliyoko karibu na eneo la tukio amesema wanawapatia matibabu watu wanne waliojeruhiwa katika maporomoko hayo ya udongo.

Matukio kadhaa ya aina hiyo yameshawahi kuikumba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo mwezi Mei mwaka 2010 maporomoko ya udongo yalikumba kijiji cha Kibiriga mashariki mwa nchi hiyo na kuua watu 19. Maiti za watu wengine 27 waliotoweka hazikupatikana.

Kijiji cha uvuvi cha Tora kilichokumbwa na maporomoko ya udongo

Aidha mwezi Februari mwaka 2002, watu 50 walipatikana wamekufa baada ya wimbi la tope na majabali kuukumba mji wa mashariki wa Uvira za kudidimiza nyumba zipatazo 150.

Tukio la maporomoko ya udongo katika mkoa wa Ituri Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limejiri siku mbili tu baada ya mji wa Regent nchini Sierra Leone kukumbwa na maafa kama hayo ambapo watu wasiopungua 400 wamefariki dunia na mamia ya wengine hawajulikani waliko.

Janga hilo la kimaumbile lililoikumba Sierra Leone limetajwa kuwa kubwa zaidi kuwahi kulikumba bara la Afrika katika miaka ya hivi karibuni…/