Upinzani Kenya wawasilisha mashtaka mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu
Muungano wa upinzani nchini Kenya wa National Super Alliance (NASA) umewasilisha kesi ya kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 8 Agosti na kufuatiwa na malalamiko na machafuko.
Muungano wa NASA unasema, matokeo ya uchaguzi huo yalichakachuliwa kwa maslahi ya mgombea wa chama cha Jubilee, Uhuru Kenyatta.
Matokeo rasmi yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) yameonesha kuwa, Uhuru Kenyatta aliyegombea kwa tiketi ya chama cha Jubilee alipata ushindi baada ya kujizolea kura zaidi ya milioni nane na laki mbili sawa na asilimia 54.27 ya kura zote, huku Raila Odinga aliyegombea kwa tiketi ya ODM akipata kura zaidi ya milioni 6 na laki saba, sawa na asilimia 44.74 ya kura zote. Hata hivyo viongozi wa NASA wanadai kuwa, Odinga alipata kura zaidi ya milioni nane huku Rais Kenyatta aliyewania kiti hicho kwa muhula wa pili akipata kura milioni saba na laki saba.
Hata hivyo kambi ya upinzani ya NASA inasisitiza kuwa, matokeo ya uchaguzi huo yalipangwa tangu awali na kwamba komputa zilizotumiwa kwa ajili ya kuhesabu kura za wananchi zilidukuliwa. Kwa msingi huo Johnson Muthama wa muungano wa upinzani anasema: NASA inawahakikishia wananchi kwamba ina azma na uwezo wa kulinda kura zao na kuhakikisha zinahesabiwa.
Baada ya kutangazwa matoke ya kura za uchaguzi wa rais yaliyoonesha kwamba kinara wa upinzani Raila Odinga ameshindwa, maelu ya wafuasi wake walimiminika mitaani wakipinga matokeo hayo. Hadi sasa watu wasiopungua 11 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika machafuko hayo. Mrengo wa upinzani nchini Kenya umedai kwamba, jeshi la polisi nchini humo limeua watu mia moja tangu yalipoanza maandamano ya kulalamikia ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa rais. Hata hivyo mrengo huo haujatoa ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.
Maafsa wa serikali ya Kenya na jamii ya kimataifa wanasisitiza kuwa wapinzani wa matokeo ya uchaguzi mkuu nchini humo wanapaswa kuheshimu demokrasia na kufuatilia matakwa yao kwa njia za kisheria. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alikuwa miongoni mwa shakhsia mbalimbali duniani waliowataka vinara wa muungano wa upinzani kufuata mkondo wa sheria kwa ajili ya kuchunguza mvutano uliosababishwa na matokeo ya uchaguzi huo.
Ingawa ghasia na machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka huu yamepungua kwa kiasi kikubwa lakini bado kuna wasiwasi wa kuibuka tena ghasia hizo iwapo pande huzika hazitatumia busara na hekima kushughulikia tatizo hilo. Kenya ina tajiriba na uzoefu mchungu wa machafuko na mauaji ya baada ya uchaguzi mkuu. Raila Odinga ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa Uhuru kenyatta katika uchaguzi wa mwaka huu wa rais aligombea kiti hicho kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa mwaka 1997 na hii ilikuwa mara ya nne kwa mwanasiasa huyo kuchuana kwa ajili ya kuingia Ikulu ya Nairobi bila ya mafanikio. Katika uchaguzi wa mwaka 2007 Raila Odinga na mrengo wake walidai kwamba, kulifanyika udanganyifu mkubwa katika matokeo ya uchaguzi, suala mbalo lilizusha machafuko makubwa kote nchini Kenya. Zaidi ya watu 1200 waliuawa katika machafuko hayo na malaki ya wengine walilazimika kuwa wakimbizi.
Wasiwasi wa kutokea machafuko na ghasia nchini Kenya iwapo wanasiasa hawatakuwa macho na makini unapata maana kwa kuzingatia muundo wa kikabila wa siasa za Kenya ambao umekuwa na nafasi na ushawishi mkubwa katika masuala muhimu kama chaguzi za rais Bunge la kadhalika. Hali hii inatiwa nguvu kwa kutazama maeneo ambayo yamekumbwa na machafuko zaidi baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais wa Kenya ambayo mengi ni ya watu wa kabila la Luo la kinara wa upinzani, Raila Odinga.
Alaa kulli hal, Uhuru Kenyatta ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa Rais wa Kenya wakati nchi hiyo ikikabiliwa na changamoto kadhaa, kubwa zaidi ikiwa ni tishio la kundi la kigaidi la al Shabab kwa usalama na maisha ya raia wa nchi hiyo. Mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi hilo pia yameathiri sana sekta ya utalii ambayo inahesabiwa kuwa miongozi mwa nguzo kuu za uchumi wa Kenya.
Inatarajiwa kuwa Wakenya wa kambi zote wataikitia wito wa busara na mantiki na kujiepusha na machafuko, ghasia na chuki za kikabila ambazo jeraha na maumivu yake yangali yanahisika baada ya machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Vilivile tunapaswa kupongeza hatua ya kinara wa kambi ya upinzani ya kuamua kufuatilia malalamiko ya kambi hiyo kwa njia za kisheria suala ambalo linatia matumaini kwamba, mvutano huo utatatuliwa kwa njia za amani hasa kwa kutilia maanani kwamba, awali Odinga alikuwa amesema kuwa hatawasilisha mashtaka mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu.