Vyama 32 vya siasa barani Afrika vyakutana mjini Khartoum, Sudan
Wawakilishi wa vyama 32 vya siasa vya nchi za Afrika wamekutana katika mji mkuu wa Sudan Khartoum kujadili njia za kustawisha uhusiano wa kisiasa barani humo.
Akihutubia ufunguzi wa kongamano la tatu la Mkutano Mkuu wa Baraza la Vyama vya Siasa vya Afrika (CAPP), Waziri Mkuu wa Sudan Bakri Hassan Salih ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za dhati za kupatikana umoja baina ya mataifa ya Afrika.
Aidha amezihimiza nchi za Kiafrika kuimarisha kambi zao za ndani kukabiliana na Ubeberu na Ukoloni Mamboleo.
Mwenyekiti wa CAPP Davies Mwila amesema mkutano huo umefanyika huku kukiwepo hali mbaya katika bara la Afrika ikiwemo migogoro ya kisiasa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Katika mkutano huo wa Khartoum, washiriki wanatazamiwa kumchagua mwenyekiti mpya wa Baraza la Vyama vya Siasa vya Afrika, Naibu Mwenyekiti na wajumbe wa kamati ya utendaji ya baraza hilo.
CAPP iliasisiwa mwaka 2013 mjini Khartoum, Sudan kwa madhumuni ya kuimarisha ushirikiano wa kisiasa na umoja baina ya nchi za Afrika.../