Safari ya Waziri Mkuu wa Libya nchini Sudan
Fayez al Sarraj Waziri Mkuu wa Libya anayeongoza serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo leo Jumapili anaelekea ziarani nchini Sudan.
Fayez al Sarraj ambaye anaongoza serikali hiyo ambayo pia inatambuliwa rasmi na jamii ya kimataifa akiwa ziarani huko Sudan mbali na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa nchi hiyo atasaini pia mikataba kadhaa ya ushirikiano na viongozi wa Khartoum. Mkataba wa kuasisi kamati ya pamoja ya mashauriano ya kisiasa kati ya Wizara za Mambo ya Nje za Sudan na Libya ni miongoni mwa nyaraka zitakazosainiwa katika safari hiyo.
Kuchunguzwa matukio ya hivi karibuni huko Libya na khususan matokeo ya mazungumzo ya hivi majuzi kati ya Rais Omar al Bashir wa Sudan na Jenerali ya Khalifa Haftar anayesimamia eneo la mashariki mwa Libya, ni maudhui nyingine zitakazojadiliwa katika ziara ya Waziri Mkuu wa Libya huko Sudan.
Serikali ya Sudan katika miaka ya karibuni imefanya mashauriano mbalimbali na vyama na serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya ili kuandaa mazingira ya kufanyika mazungumzo ya kisiasa kati ya makundi hasimu huko Libya. Serikali ya Sudan inaitambua rasmi serikali ya umoja wa kitaifa inayoongozwa na Fayez al Sarraj, hata hivyo wakati huo huo ina uhusiano wenye mivutano kati yake na Jenerali Khalifa Haftar. Makundi ya wanamgambo katika nchi mbili hizo pia yana mahusiano yenye mvutano. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa waasi wengi wa Sudan ambao ni kutoka katika jimbo la Darfur magharibi mwa nchi hiyo wamejiunga na wapiganaji wa Khalifa Haftar wakipigana bega kwa bega upande wa jenerali huyo. Hii ni katika hali ambayo viongozi wa Sudan nao pia wanadai kuwa makundi ya Libya yanawaunga mkono kikamilifu waasi wa Darfur na kuwatumia zana za kijeshi, silaha na bidhaa za chakula.
Japokuwa huko nyuma Abdulwahid Yusuf Gavana wa jimbo la Darfur ya Kaskazini alitangaza kuwa wanajeshi wa Sudan wameingia eneo hilo ili kuwaongezea nguvu wanajeshi walioko katika mipaka ya pamoja kati ya nchi hiyo na Libya.
Katika upande mwingine, magendo ya binadamu na kuwepo magenge ya biashara hiyo katika mipaka ya nchi mbili hizo ni suala jingine linalozitia nchi hizo wasiwasi. Kitambo nyuma televisheni ya al Jazeera iliripoti kuwa: Sudan ina wasiwasi na hali ya usalama katika mipaka yake na Libya. Aidha Sudan ina wasiwasi kuhusu usalama wa mipaka kati yake na Libya na vile vile usalama wa eneo la pande tatu za Chad, Sudan na Libya.
Mashauriano ya kuhitimisha mgogoro wa kisiasa huko Libya yangali yanaendelea ambapo juhudi zilizofanywa hadi sasa hazijazaa matunda. Kuwepo makundi mawili yanayotawala huko Libya si tu yameipelekea nchi hiyo kuyumba kisiasa, bali pia hivi sasa hali ya mambo ya nchi imekuwa ya mashaka zaidi kufuatia kurejea nchini wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh na kuathiriwa pia na hali mbaya ya kibinadamu. Katika mazingira hayo, nchi za Magharibi na baadhi ya nchi katika eneo zinaendelea kushirikiana na waitifaki wao ili kuingilia masuala ya ndani ya Libya. Katika hali kama hiyo, uungaji mkono wa Saudia na umoja uliopo kati ya Sudan na nchi hiyo unapasa kuzingatiwa katika safari inayoanza leo ya Waziri Mkuu wa Libya huko Sudan. Fayez al Sarraj Waziri Mkuu wa Libya anaungwa mkono na Imarati, Misri na Saudi Arabia huku nchi hizo zikiitambua Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri kuwa adui wao. Kwa msingi huo mazungumzo kati ya Jenerali Haftar na viongozi wa Sudan na kutiwa saini makubaliano ya ushirikiano kati ya pande mbili hizo pia yanapaswa kutathminiwa katika uwanja huo.