Mahakama ya Misri yawahukumu kifungo cha maisha watu 25
Mahakama nchini Misri imewahukumu watu 25 kifungo cha maisha jela kwa tuhuma za kuhusika na matukio ya utumiaji mabavu ya mwaka 2015 nchini humo.
Mahakama ya jinai ya mji wa Damanhur makao makuu ya mkoa wa Beheira nchini Misri ilitoa hukumu hiyo jana dhidi ya watuhumiwa 25 akiwemo Halmi Abu Kashik, mmoja wa viongozi wakubwa wa harakati ya Ikhwanul Muslimin ambaye awali maafisa wa Cairo walitangaza kuwa aliuawa katika ufyatulianaji risasi na askari wa usalama. Hukumu hiyo iliyotolewa jana ni ya hatua ya mwanzo na inaweza kupingwa katika mahakama ya juu kabisa ya rufaa ya nchi hiyo.
Tangu alipoondolewa madarakani Muhammad Mursi, rais wa zamani wa Misri aliyechaguliwa na wananchi mwaka 2012, mamia ya wafuasi wa kiongozi huyo wamekwishahukumiwa vifungo tofauti vikiwemo vya maisha jela, huku wengine pia wakihukumiwa adhabu ya kifo na mahakama za nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Umoja wa Mataifa umezitaja hukumu hizo kuwa hazijawahi kushuhudiwa katika historia ya sasa. Aidha serikali ya sasa ya Rais Abdel Fattah el-Sisi inatajwa kuwa ya kidikteta na kandamizi dhidi ya wapinzani.