Somalia yakataa "rushwa" ya Saudia, yagoma kujiunga na nchi zinazoisusia Qatar
(last modified Thu, 31 Aug 2017 02:53:43 GMT )
Aug 31, 2017 02:53 UTC
  • Somalia yakataa

Rais wa Somalia amekataa pendekezo la kupewa Euro milioni 68 lililotolewa na utawala wa Kifalme wa Saudi Arabia mkabala wa kujiunga na muungano wa nchi zilizokata uhusiano wao na kuisusia Qatar.

Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia jana Jumatano alikataa pendekezo la Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudi Arabia la kujiunga na muungano wa nchi kadhaa za Kiarabu zilizoisuia Qatar na kuiwekea vikwazo na badala yake Rais wa Somalia ametoa wito wa kutatuliwa mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo.

Ripoti ya tovuti ya Gulf Times imesema kuwa, mbali na kupinga mashinikizo hayo dhidi ya Qatar, Somalia pia imeziruhusu ndege za nchi hiyo kutumia ardhi na anga ya Somalia kwa ajili ya safari za kimataifa. 

Kufuatia msimamo huo wa Somalia, serikali ya Imarati imezidisha harakati zake hasi katika maeneo yanayojitawala ya Somaliland na Puntland ambayo serikali ya Mogadishu inasisitiza kuwa ni milki na ardhi yake. 

Mfalme Salman wa Saudi Arabia

Saudia pamoja na nchi tatu za Kiarabu wapambe wake zilikata uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar kwa tuhuma kwamba nchi hiyo inaunga mkono ugaidi na haifuati sera za Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi linaloongozwa na Riyadh katika mahusiano yake ya kigeni. Qatar inakadhibisha madai ya kuunga mkono ugaidi na inasisitiza kuwa, ni nchi inayojitawala na kamwe haitafuata siasa za kiimla za Saudia. 

Tags