Mwanasheria Mkuu wa Chadema Tanzania, apigwa risasi na watu wasiojulikana
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34033-mwanasheria_mkuu_wa_chadema_tanzania_apigwa_risasi_na_watu_wasiojulikana
Mbunge wa Singida Mashariki, Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu amevamiwa na watu wasiojulikana na kupigwa risasi kadhaa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 07, 2017 09:43 UTC
  • Mwanasheria Mkuu wa Chadema Tanzania, apigwa risasi na watu wasiojulikana

Mbunge wa Singida Mashariki, Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu amevamiwa na watu wasiojulikana na kupigwa risasi kadhaa.

Tukio hilo limetokea leo wakati Lissu alipokuwa nyumbani kwake mjini Dodoma ambapo watu hao walimvamia akiwa kwenye gari lake  na kuanza kumpiga risasi za miguuni na tumboni. Habari zaidi zinaeleza kuwa, Tundu Lissu alikuwa akitokea Bungeni na alienda nyumbani kwa ajili ya kula chakula cha mchana.

Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki, Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kuwa, hali ya mwanasiasa huyo ni mbaya na kwamba amepelekwa katika chumba cha upasuaji katika hospitali ya rufaa mjini Dodoma. Viongozi mbalimbali wa kisiasa wamefika katika hospitali hiyo ili kujua maendeleo ya mwanasheria huyo ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa akiikosoa vikali serikali ya Tanzania. Kwa mujibu wa habari baadhi ya ndugu na wanasiasa wamefurika katika chumba alikolazwa huku wakigoma kutoka nje kutokana na kile walichosema kuwa hawamwamini mtu yeyote, ingawa mganga mkuu wa mkoa wa Dodoma, Charles Kihologwe, amewataka watu hao kukaa mbali na chumba hicho.

Gari iliyokuwa ikitumiwa na Tundu Lissu

Asubuhi ya leo Lissu alihudhuria kikao cha bunge ambapo pia aliomba mwongozo wa Naibu Spika akihoji juu ya taarifa za kamati zilizoundwa na Spika wa bunge Job Ndugai kwa ajili ya kutathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya Tanzanite na almasi nchini Tanzania.