UNESCO: Watoto milioni 1.8 wamenyimwa fursa ya kusoma Sudan Kusini
Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO limetangaza kuwa, watoto wapatao milioni 1.8 wamenyimwa fursa ya kusoma katika nchi ya Sudan Kusini kutokana na hali mbaya ya vita na ukosefu wa amani.
Ofisi ya UNESCO nchini Sudan Kusini imetangaza kuwa, watoto katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika wanakabiliwa na hali mbaya likiwemo suala la kukosa fursa ya kwenda shule kutokana na ukosefu wa usalama.
Kwa mujibu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO ni kuwa, hali ya kielimu katika nchi hiyo ni mbaya. Aidha taarifa ya UNESCO imeongeza kuwa, licha ya kuweko juhudi za serikali ya Juba na asasi za kimataifa kwa ajili kuwapatia elimu watu, lakini kiwango cha watu wasiojua kusoma na kuandika bado hakiridhishi katika nchi hiyo.
Sehemu nyingine ya ripoti ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO iliyotolewa kwa mnasaba wa tarehe 8 Septemba ambayo ni siku ya kimataifa ya kupiga vita ujinga wa kutojua kusoma na kuandika inaeleza kuwa, ni asilimia 4 tu ya walimu huko Sudan Kusini ambao wana elimu ya Chuo Kikuu.
Wakati huo huo, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO limetangaza kuwa, kuna watu milioni 750 ambao ni wajinga wa kutojua kusoma na kuandika kote ulimwenguni.
Jana walimwengu waliadhimisha siku ya kimataifa ya kuupiga vita ujinga wa kutokujua kusoma na kuandika. Siku hii ambayo huadhimishwa kila mwaka hutoa fursa ya kutathmini hatua zilizopigwa na kuchukua hatua kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.