Mkutano wa utawala wa Kizayuni wa Israel na nchi za Afrika waakhirishwa
Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala wa Kizayuni wa Israel imetangaza kuwa mkutano wa utawala huo na nchi za Afrika uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi ujao nchini Togo umeakhirishwa hadi wakati mwengine.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imetangaza kupitia taarifa kwamba uamuzi huo umechukuliwa na Rais Faure Gnassingbe wa Togo baada ya mashauriano aliyofanya na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Pasi na kuashiria sababu ya kuakhirishwa mkutano huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imeeleza kwamba mazungumzo yataendelea kufanywa ili kufanikisha kufanyika kwa mkutano huo katika siku zijazo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina, lengo la mkutano huo ni kuimarisha uhusiano wa Israel na Afrika; na invayoonekana kuakhirishwa kwake kumetokana na mashinikizo ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na baadhi ya nchi za Kiarabu na zisizo za Kiarabu.
Ripoti aidha zinaeleza kuwa Rais Faure Gnassingbe wa Togo ambaye hivi sasa anakabiliwa na mashinikizo ya upinzani wa ndani unaomtaka angátuke madarakani amemueleza Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu kwamba ameghairi kuwa mwenyeji wa mkutano wa Israel na nchi za Afrika kwa sababu ya hali ya ndani ya nchi yake.
Hapo kabla nchi kadhaa za Afrika zilikuwa zimeshatangaza kuwa zitasusia kushiriki mkutano huo wa Togo. Miongoni mwao ni Afrika Kusini ambayo imesema kushiriki mkutano huo ni sawa na kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel na imezitaka nchi nyengine pia kuchukua hatua hiyo.
Nchi nyengine za Afrika zilizotangaza msimamo wa kususia mkutano wa Israel na nchi za Afrika ambao ulipangwa kufanyika tarehe 23 na 24 za mwezi ujao wa Oktoba nchini Togo ni Morocco, Algeria, Tunisia, Mauritania na Sudan.../