Kura zahesabiwa baada ya uchaguzi Zanzibar
Zoezi la kuhesabu kura linaendelea visiwani Zanzibar baada ya uchaguzi kufuatia matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015 kufutwa na tume ya uchaguzi ya visiwa hivyo ZEC.
Mgombea wa Chama cha Mapinduzi CCM Dkt Ali Mohammed Shein alipiga kura yake katika kituo cha Bungi, Kibera katika kisiwa cha Unguja. Chama cha Wananachi CUF kilitoa wito kwa wafuasi wake kususia uchaguzi wa leo. Chama hicho kinaamini kilishinda uchaguzi uliofanyika mwaka jana na mgombea wake Maalim Seif Hamad anafaa kutangazwa mshindi.
Mgombea urais wa chama cha ADC Hamad Rashid amepiga kura yake kituo cha Tondooni Wawi wilaya ya Chake-Chake, mkoa wa Kusini Pemba. Amesema: "Nina imani ya kuwa Rais, nikikosa nitakuwa Makamu wa Rais".
Usalama ulimarishwa visiwani Zanzibar na maafisa wa usalama walionekana wakilinda doria katika maeneo yote ya Unguja na Pemba. Kuna watu takribani 500,000 waliojiandikisha kupiga kura Zanzibar katika uchaguzi ambapo wanatazamiwa kumchagua rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani. Idadi ya wapiga kura waliojitokeza ni wachache ikilinganishwa na uchaguzi wa Oktoba 25.