Chaguzi sita zafanyika Afrika leo
Leo kumekuwa na upigaji kurakatika nchi sita za Afrika yaani nchini Kongo Brazzaville, Benin, Niger, Cape Verde, Visiwani Zanzibar nchini Tanzania na kura ya maoni nchini Senegal.
Nchini Senegal raia wanapiga kura kuamua iwapo kipindi cha kuhudumu kwa rais kitasalia kuwa miaka saba au kipunguzwe kuwa miaka mitano.
Jamhuri ya Kongo inafanya uchaguzi wake wa duru ya kwanza wa Urais ambako kuna wagombea tisa akiwemo rais wa sasa Sassou Nguesso.
Benin na Niger zinafanya duru ya pili ya uchaguzi wa urais, huku nayo Zanzibar ikirudia uchaguzi baada ya matokeo ya kwanza kufutwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ukiukwaji wa taratibu.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma ametoa wito wa kufanyika kwa njia ya amani uchaguzi pamoja na kura ya maoni kwenye nchi hizo sita barani Afrika hivi leo.
Amesema wakati tume za uchaguzi zikiendesha shughuli zao kwa njia ya kitalaamu wananchi na wadau wa kisiasa wanafaa kuheshimu matokeo ya kura na kuwasilisha malalamiko kwa njia zinazoendana na katiba.