Tarehe ya uchaguzi wa marudio Kenya yasogezwa mbele
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34693-tarehe_ya_uchaguzi_wa_marudio_kenya_yasogezwa_mbele
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) imebadilisha tarehe ya kufanyika uchaguzi wa marudio wa urais hadi Oktoba 26 mwaka huu na wala sio Oktoba 17 kama ilivyotangaza hapo awali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 22, 2017 04:22 UTC
  • Tarehe ya uchaguzi wa marudio Kenya yasogezwa mbele

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) imebadilisha tarehe ya kufanyika uchaguzi wa marudio wa urais hadi Oktoba 26 mwaka huu na wala sio Oktoba 17 kama ilivyotangaza hapo awali.

Taarifa ya IEBC iliyosainiwa na Mwenyekiti, Wafula Chebukati imesema uamuzi huo umefikiwa ili kuipa tume hiyo muda wa kujiandaa zaidi na hasa katika masuala ya teknolojia.

Chebukati amesema kama tunavyomnukuu, “Ili kuhakikisha tume inajiandaa kuleta uchaguzi wenye viwango vinavyohitajika na Mahakama ya Juu, tunapenda kuujulisha umma na wadau wote kuwa uchaguzi mpya utafanyika siku ya Alkhamisi tarehe 26 mwezi Oktoba mwaka huu 2017.”

Baraza la Mawaziri hapo jana liliidhinisha bajeti ya Shilingi bilioni 10 za Kenya zitakazotumiwa katika zoezi hilo.

Majaji wa Mahakama ya Juu Kenya

Mahakama ya Juu ya Kenya iliamuru uchaguzi wa marudio ufanyike ndani ya muda wa siku 60 kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa mrengo wa upinzani NASA Raila Odinga ambaye aliyapinga matokeo ya uchaguzi wa rais wa Agosti 8 katika mahakama hiyo.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya ilikuwa imemtangaza Rais Kenyatta mshindi, kwa kumpiku Odinga kwa kura zaidi ya milioni moja na laki nne.

Rais Kenyatta na Odinga watakaochuana Oktoba 26

Uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Kenya kubatilisha ushindi wa rais uliotangazwa tarehe Mosi ya mwezi huu wa Septemba ulikuwa wa kwanza kutolewa barani Afrika na wa nne kote duniani.