Somalia yakerwa na hatua ya Galmudug kukata uhusiano na Qatar
Serikali kuu ya Somalia imekosoa vikali hatua ya eneo lenye mamlaka ya ndani la Galmudug kutangaza kuwa linaziunga mkono Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu katika mgogoro wa nchi za Kiarabu.
Taarifa ya serikali ya Mogadishu imesema msimamo uliotangazwa na Galmudug Jumatano iliyopita wa kujiunga na maeneo mengine mawili yenye mamlaka ya ndani ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, yaani Puntland na Hirshabelle 'kusimama na Saudia na Imarati' hauna taathira, kwani Serikali ya Federali ya nchi hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kutoa kauli ya mwisho ikija katika masuala ya sera za kigeni.
Taarifa hiyo imesema maeneo yenye mamlaka ya ndani ya nchi hiyo yanafaa kuchukua msimamo wa wastani katika mgogoro huo.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Agosti, Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia alikataa kupokea 'rushwa' ya Euro milioni 68 ili kuunga mkono pendekezo la Mfalme Salman bin Abdulaziz wa Saudi Arabia la kujiunga na muungano wa nchi kadhaa za Kiarabu zilizoisusia Qatar na kuiwekea vikwazo na badala yake Rais wa Somalia alitoa wito wa kutatuliwa mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo.
Juni 5 mwaka huu Saudia pamoja na nchi tatu za Kiarabu wapambe wake zilikata uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar kwa tuhuma kwamba nchi hiyo inaunga mkono ugaidi na haifuati sera za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi linaloongozwa na Riyadh katika mahusiano yake ya kigeni.
Qatar inakadhibisha madai ya kuunga mkono ugaidi na inasisitiza kuwa, ni nchi inayojitawala na kamwe haitafuata siasa za kiimla za Saudia.