UN yaafiki kuendelea na uchunguzi wake kuhusu Burundi
-
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi
Tume ya haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa leo Ijumaa imepitisha azimio jipya kuhusu nchi ya Burundi baada ya uchunguzi uliobaini kuwa mauaji, utesaji na ukamataji wa raia umekuwa ukiendelea nchini humo.
Azimio hilo liliwasilishwa dakika za mwisho mbele ya tume hiyo ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya haki za binadamu na kundi la wataalamu kutoka bara la Afrika, ambao walitembelea mji mkuu wa Burundi, Bujumbura ambako walikusanya ripoti nyingi kuhusu kupotea watu, mauaji ya kiholela na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini humo.
Azimio hili limependekeza kutumwa timu mpya ya wataalamu watatu wa umoja wa mataifa wa haki za binadamu ambao watashirikiana na wakuu wa serikali ya Bujumbura kuchunguza visa vya uhalifu dhidi ya binadamu, mauaji na unyanyasaji unaodaiwa kufanyika nchini humo.
Kumekuwa na hali ya vuta nikuvute kati ya serikali ya Bujumbura na tume ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu kuhusu ripoti iliyotolewa hivi karibuni ikibainisha kuendelea vitendo vya mauaji, udhalilishaj, na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Burundi.
Wakati huo huo shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International limeonya kuwa Maelfu ya wakimbizi wa Burundi wanaorejea nyumbani nchini Tanzania wanakabiliwa na hatari za kiusalama nchini mwao.
Mwezi uliopita, Tanzania, Burundi na shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi UNHCR walikubaliana kwamba kufikia mwisho wa mwaka huu wawe wamewarejesha wakimbizi elfu kumi na mbili wanaoishi Tanzania na wanaotaka kurudi kwao Burundi kwa hiari.
Lakini Amnesty International inasema, mpango huu unahatarisha maisha ya maelfu ya wakimbizi na inaamini kuwa wakimbizi wengi wanarejeshwa nyumbani kwao kutokana na mashinikizo ya serikali za Tanzania na Burundi.
Burundi ilitumbukia katika machafuko mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza, kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mara ya tatu mfululizo, machafuko ambayo yalishika kasi zaidi mjini Bujumbura. Wapinzani waliitaja hatua ya Rais Nkurunziza kushiriki katika uchaguzi huo kwamba ilikiuka katiba na hati ya makubaliano ya amani ya Arusha Tanzania lakini serikali ya Bujumbura imesema haijakiuka sheria.