Uturuki yafungua kituo chake kikubwa cha kijeshi nchini Somalia
(last modified Sun, 01 Oct 2017 06:43:38 GMT )
Oct 01, 2017 06:43 UTC
  • Uturuki yafungua kituo chake kikubwa cha kijeshi nchini Somalia

Uturuki imefungua kituo chake kikubwa zaidi cha kijeshi barani Afrika ambacho kiko katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Kituo hicho kilifunguliwa jana Jumamosi katika sherehe iliyohudhuriwa na Mkuu wa Majeshi ya Uturuki Jenerali Hulusi Akar na Waziri Mkuu wa Somalia Hassan Ali Khayre.

Kituo hicho cha kijeshi kitakuwa pia ni chuo cha mafunzo kwa askari wa Somalia ambapo kutakuwa pia na maafisa 200 wa kijeshi wa Uturuki watakaokuwa na jukumu la kutoa mafunzo hayo.

Akizungumza katika ufunguzi wa kituo hicho, Khayre ameipongeza Uturuki kwa uungaji mkono wake usioterereka kwa Somalia wakati nchi hiyo ikiwa katika mkakati wa kuanzisha jeshi imara kukabiliana na magaidi. Mwaka jana pia Uturuki ilifungua ubalozi wake mjini Mogadishu ambao umetajwa kuwa mkubwa zaidi wa nchi hiyo duniani.

Wanajeshi wa Somalia wakiungwa mkono na askari 22,000 wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika wamefanikiwa kutoa pigo kwa magaidi wa al Shabab.

Pamoja na hayo magaidi hao wenye uhusiano na mtandao wa al Qaeda wangali wanaendelea kufanya hujuma za kuvizia Somalia na pia katika nchi jirani ya Kenya. 

Jeshi la Somalia linatazamiwa kuchukua udhibiti kamili wa usalama nchini humo baada ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika kuondoka katika muda uliopangwa.

Tags